Monday, August 3, 2009

FISADI MKUU TANESCO DR IDRIS RASHID




MBUNGE wa Sumve (CCM), Richard Ndasa ameibua ufisadi katika Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kulieleza Bunge kuwa shirika hilo liko katika harakati ya kuiuza kwa Sh60 milioni nyumba namba 13 iliyoko Oysterbay jijini Dar es Salaam, Mtaa wa Toure/ Chaza line baada ya kuikarabati kwa Sh600 milioni.


Sambamba na ufisadi huo, pia Shirika hilo linatuhumiwa kutumia Sh1.4 bilioni kukarabati nyumba sita za wakurugenzi kinyume na taratibu.

Ndasa alitoa tuhuma hizo nzito bungeni jana alipokuwa akichangia bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini iliyowasilishwa Jumamosi iliyopita na waziri wake, William Ngeleja.

Ndasa alisema fedha hizo ambazo ni sehemu ya mkopo wa Sh280 bilioni iliyochukuliwa benki kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maendeleo ya Tanesco, imetumika bila idhini ya bodi ya wakurugenzi.


"Tanesco kuna matatizo makubwa yanayotokana na usimamizi mbovu na matumizi mabaya ya fedha. Shirika halina vipaumbele, linatumia vibaya fedha za umma," alisema Ndasa na kuongeza:"Mwaka 2007 shirika hilo lilikopa Sh280 bilioni kutoka benki mbalimbali kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lakini badala ya kutekeleza vipaumbele, limeamua kukarabati nyumba za wakubwa kwa zaidi ya Sh1.4 bilioni".


Mbunge huyo alitaja nyumba zingine zilizofanyiwa ukarabati huo na gharama zake kwenye mabano kuwa ni namba 89 iliyoko Barabara ya Guinea (Sh250,463,140), namba 65 iliyoko Barabara ya Lisbon (Sh 190,407,430) na namba 159 iliyoko mtaa wa Mawenzi iliyokarabatiwa kwa Sh130 milioni.


Nyingine ni nyumba namba 93 Barabara ya Guinea (Sh 88,515,820), namba 315, Mtaa wa Toure Drive ( Sh79 milioni) na namba 98 iliyoko katika Barabara ya Uganda iliyokarabatiwa kwa zaidi ya Sh730 milioni.


"Bodi ya wakurugenzi haikuidhinisha matumizi ya fedha hizo," alisema Ndasa ambaye pia alifafanua kuwa mkopo wa fedha hizo utatakiwa kurudishwa na wananchi kupitia bili za umeme.


Akizungumza nje ya Ukumbi wa Bunge, Ndasa alifafanua kuwa nyumba namba 13 iliyoko Oysterbay iliyokarabatiwa kwa zaidi ya Sh600 milioni, inakaliwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Dk Idris Rashid ambaye amebakisha miezi mitatu kumaliza mkataba wake wa miaka mitatu, ametuhumiwa kujipangia kuinunua kwa Sh 60 milioni.


Kimahesabu nyumba hiyo itakuwa imeuzwa kwa asilimia 10 ya thamani ya kuikarabiti, mbali na thamani yake halisi pamoja na gharama za kiwanja hicho kilichoko eneo la Oysterbay ambayo ni ghali.


Kwa mujibu wa Ndasa, matumizi hayo ya fedha za mkopo unaopaswa kurejeshwa kwa kiasi cha Sh4 bilioni kila mwaka kuanzia mwakani, ni mabaya na ndiyo yanayochangia shirika hilo kushindwa kusambaza umeme vijijini.


Kauli ya Ndasa iliungwa mkono na Mbunge wa Busega Raphael Chegeni (CCM), aliyelieleza Bunge kuwa Tanesco inapitia misukosuko ya mfumo wa kiutendaji.


Alisema shirika hilo ambalo Watanzania waliamini uongozi mpya ungewasaidia baada ya kuondolewa kwa kampuni ya Net Group Solutions ya Afrika Kusini, lina matatizo makubwa ya usimamizi wa fedha na vipaumbele.


"Wakati tunaifukuza Net Group Solutions tulijua sasa tumemaliza tatizo, kumbe ovyo. Tumeshuhudia Tanesco ikipitia misukosuko mingi ya kimfumo na utendaji na kuonekana kuwa na tatizo kubwa la usimamizi wa fedha," alisema na kuongeza:"Mimi naomba katika bajeti hii tuangalie tunabadilishaje mfumo huu. Tunahitaji kujua lini Tanesco itamalizia miradi ya umeme vijijini.Tutakuzaje uchumi kama nchi haina umeme?".


Naye Mbunge wa Ukerewe, Dk Getrude Mongela (CCM) aliwataka wafanyakazi wa Tanesco kuongeza kasi ya utendaji ili shirika likamilishe miradi ya umeme vijijini.


"Wafanyakazi Tanesco acheni uzembe, we are serious (hatutaki mzaha) kwani hata kama hamna fedha; hizo kidogo mlizonazo mnaweza kuzitumia vizuri na kwa uangalifu zikaleta matunda yaliyokusudiwa," alisema Mongela.


Hata hivyo, alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo nje ya Ukumbi wa Bunge, Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Dk Idris Rashid aligoma akisema, "Haya ni masuala ya Bunge atayajibu waziri". Alipoulizwa zaidi kwamba, haoni tuhuma hizo zimeelekezwa kwake moja kwa moja alijibu kwa mkato zaidi, ”Nasema sisemi chochote, hili ni Bunge".


Mwaka juzi uongozi wa Tanesco ulisema unahitaji mabilioni ya shilingi kwa ajili ya kuboresha miundombinu ili angalau kuliweka katika hali nzuri ya kuweza kutoa huduma ya umeme nchini.

2 comments:

Anonymous said...

your welcome dude

Anonymous said...

Hii nchi imekuwa kama shamba la bibi kila mtu ankuja na kuchukua kilicho chake na kuondoka wakati asilimia 80 ya watanzania wanendlea kuwa maskini wa kutupa..

Kwa wanofuatilia habari za tz na kuchambua uwezo wa viongozi wetu, binafsi naafiki kabisa kuwa uwezo wa raisi wetu JK ni mdog na hata u,ifuatilia hotuba zake hupati cha kuandika cha maana.

Kwa mfano jana alipokuwa anahutubia wakulima katka ufunguzi wa sherehe za nane nae huwezi kuamini kuwa maneno aiyoyatoa pale alikuwa anaongea kama Rais mwenye dhamana ya juu kabisa hapa tz. Alitaja kuwa tatizo kubwa la maendeleo ya watanzania ktk kilimo , JK ametaja anasa za Watanzania kuwa moja ya mambo yanayofanya sekta ya kilimo kushindwa kufikia malengo ya kuwa uti wa mgongo kwa uchumi wa Tanzania, kwani waTZ walio wengi wananunua magari ya kifahari badala ya matraktor ya kulimia. Jiulize magari ya kifahari yanayotumia na viongozi wetu.. hvi haoni kenya wamefanyaje mpka yeye ang'ng'anie ma GX V8 kwa kila kiongozi, pesa ya hayo magari ni matraktor mangapi.. Tunakata ngapi tushindwe kupeleka matraktor?
Jamani mlioko govt tunaomba waoneeni huruma watanzania wa kawaida maskini